Mada Muhimu: Kufanywa na Kuishi kama Mwana wa Mungu, Upendo wa Baba, Toba
[Dhana Muhimu za Injili: Dhambi, Iliyoumbwa kwa Mfano wa Mungu, Urafiki wa karibu na Baba]
Siku moja watoza ushuru na wenye dhambi walikuwa wamekusanyika ili wapate kumsikiliza Yesu. Lakini Mafarisayo na walimu wa sheria wakanung’unika wakisema, “Huyu mtu anawakaribisha wenye dhambi na kula nao.” Ndipo Yesu akawaambia mifano kadhaa ikiwemo huu.
“Kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili. Yule mdogo akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Hivyo akawagawia wanawe mali yake.
“Baada ya muda mfupi, yule mdogo akakusanya vitu vyote alivyokuwa navyo, akaenda nchi ya mbali, na huko akaitapanya mali yake kwa maisha ya anasa. Baada ya kutumia kila kitu alichokuwa nacho, kukawa na njaa kali katika nchi ile yote, naye akawa hana chochote. Kwa hiyo akaenda kuajiriwa na mwenyeji mmoja wa nchi ile ambaye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Naye akatamani kujishibisha kwa maganda waliyokula wale nguruwe, wala hakuna mtu aliyempa chochote.
“Lakini alipozingatia moyoni mwake, akasema, ‘Ni watumishi wangapi walioajiriwa na baba yangu ambao wana chakula cha kuwatosha na kusaza, bali mimi hapa nakufa kwa njaa! Nitaondoka na kurudi kwa babangu na kumwambia, ‘Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili tena kuitwa mwanao.
Tafadhali nifanye tena kama mmoja wa watumishi wako.’ Basi akaondoka akaenda kwa babake.
“Lakini alipokuwa bado yupo mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu. Mwana wake akamwambia babake, ‘Baba, nimefanya dhambi mbele yako na mbele ya Mungu.
Sistahili kuitwa mwanao tena.’
“Lakini babake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana na kumvika, mkamvike pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake. Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi. Kwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena. Alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kufanya tafrija.
AYA ya KUKUMBUSHA: Wagalatia 4:4,5 - “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.”