CBS Stories

Swahili Stories

Yakobo Ashindana Mwereka na Mungu

Mwanzo 32 & 33

Baada ya Yakobo kukaa miaka mingi na Laban, alibarikiwa na makundi mengi ya wanyama wa kuchunga, na watoto wengi na watumishi wengi. Aliamua kurudi Kanaani lakini bado aliogopa kakake Esau aliyemwibia baraka yake ya Baba.

Walipokaribia nchi ya Kanani, Yakobo alizituma zawadi nyingi za wanyama kujaribu kupata fadhili kwa kakake. Wajumbe wake walirudi wakamwambia, "Esau anakuja na wanaume mia nne." Yakobo aliogopa sana, kwa hivyo aliomba, “Ee Mungu wa baba yangu Abrahamu, Mungu wa baba yangu Isaka, Eee BWANA, ambaye uliniambia, ‘Rudi katika nchi yako na jamaa yako, nami nitakufanya ustawi,’ mimi sistahili fadhili na uaminifu wako wote ulionitendea mimi mtumishi wako. Nakuomba, uniokoe na mkono wa ndugu yangu Esau. Ninaamini ahadi yako kufanya uzao wangu kuwa mwingi na kuwa hauwezi kuhesabika!’

Walipofika Mto wa Yordani, Yakobo aliwavusha wake zake na watoto wake ng’ambo ya mto, naye akarudi upande mwingine. Yakobo alikuwa peke yake. Baadaye usiku, mtu mmoja alishindana naye mweleka hadi mapambazuko. Yule mtu alipoona hashindwi akagusa nyonga ya Yakobo hivyo nyonga yake ikateguka huku akishindana na mwanaume huyo. Akasema, “Niache niende, maana kunapambazuka.” Lakini Yakobo akajibu, “Sitakuacha uende usiponibariki.”

Ndipo yule mtu akasema, “Jina lako halitakuwa tena Yakobo, bali Israeli, kwa sababu umeshindana na Mungu na watu pia nawe umeshinda.”

Yakobo akasema, "Nimemwona Mungu uso kwa uso, na hata hivyo maisha yangu yameokoka."

Malaika alipoondoka, Yakobo alimwona Esau akija na jeshi. Alimwendea akainamisha kichwa chake kwa unyenyekevu. Esau akampokea kwa huruma na msamaha akashangaa jinsi Mungu alivyombariki Yakobo na watoto na wanyama. Yakobo akampatia Esau zawadi nyingi kama kondoo, mbuzi, ng’ombe, na ngamia akisema, “Kuuona uso wako ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa kuwa umenipokea kwa neema kubwa. Tafadhali ukubali zawadi zilizoletwa kwako kwa kuwa Mungu amenineemisha na vyote nilivyohitaji.” Badaye, Yakobo na Esau waliishi kama majirani kwa miaka mingi.