CBS Stories

Swahili Stories

Wapelelezi Kumi na Wawili, Nyoka Katika Jangwani

Hesabu 13:1 – 14:12; 21:1-9

Wapelelezi Kumi na Wawili Wanaichunguza Kanaani:

Baada ya Bwana kutoa maagizo kwa Musa katika Mlima Sinai, watu walielekea Kanani kwa sababu hii ndiyo ilikuwa ahadi ambayo Mungu alimpa Abrahamu, Isaka, na Yakobo. Musa akatuma wapelelezi kumi na wawili walioenda katika nchi yote ya Kanaani kwa siku arobaini. Kusudi lao ilikuwa kupata habari ili Waisraeli wapange jinsi ya kuivamia.

Hata hivyo, wapelelezi waliporudi, wote walikubali ya kwamba ilikuwa nchi nzuri na ilikuwa ikitiririka maziwa na asali ya nyuki, lakini kumi kati yao walikuwa na ujumbe mbaya wakisema kwamba, watu wa miji huko walikuwa hodari sana na kwamba Waisraeli hawangewashinda. Lakini wapelelezi wawili, Yoshua na Kalebu, walijaribu kuwashawishi kuingia, wakiwakumbusha yale yote Mungu alikuwa amewafanyia kuwaokoa kutoka Misri, na huyo huyo Mungu angewasaidia kuwashinda adui zao.

Lakini watu waliasi wasiingie.

Kwa hivyo, Mungu alileta hukumu juu yao akitangaza kwamba hakuna yeyote aliyekuwa na miaka ishirini au zaidi kwa wakati huo, ambaye angeingia nchi ya ahadi, na kwamba Waisraeli wangezunguka jangwani kwa miaka arobaini, mwaka mmoja kwa kila siku ambayo wapelelezi walikuwa katika nchi ya Kanaani, mpaka kizazi chote kife na kwisha.

Miaka Arobaini Jangwani / Kutokuamini kwa Israeli:

Hivyo basi, Waisraeli walizurura jangwani. Musa aliwaongoza na Mungu aliwaletea chakula na maji katika njia ya ajabu. Lakini watu walikuwa wanalalamika mara kwa mara.

Wakati mmoja, walipokuwa wakizurura watu walimnung’unikia Mungu na Musa, wakisema, “Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani?

Hakuna mkate wala maji, na tunachukia sana hii mana ambayo Mungu alitupatia!”

Mungu alikasarika. Bwana akatuma nyoka za moto kati yao, wakawauma, na watu wengi wakafa. Watu wakamwendea Musa, wakasema, “Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa BWANA, ili atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu.

Bwana akamwambia Musa, “Jifanyie nyoka wa shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu atakayeumwa, aitazamapo ataishi.” Musa akafanya nyoka wa shaba, na kumweka juu ya mti. Baadaye, wakati mtu yeyote alipoumwa na nyoka, akimtazama yule nyoka wa shaba aliishi.

Lakini mwenendo kama huu ulikuwa kawaida kwa kizazi hicho cha Waisraeli. Basi walizurura jangwani kwa miaka arobaini kama Mungu alivyosema.

Kuingia katika Nchi ya Ahadi:

Mwishowe, baada ya miaka arobaini katika jangwa, Mungu aliwaleta Waisraeli mpakani wa nchi ya ahadi. Akawaambia Waisraeli hivi,

  1. Moja, msiabudu miungu mingine au kuiinamia sanamu kamwe!
  2. Pili, msiwe na Mungu hawapi nchi hii kwa sababu ya wema wenu. Ndiyo nyinyi ni watu wa shingo ngumu. Ninawatumia nyinyi kuwaadhibu mataifa kwa sababu ya maovu yao.
  3. Tatu, Mungu anawapatia nchi hii kwa sababu anawapenda na anatimiza ahadi ambayo aliwafanyia Abrahamu, Isaka, na baba wenu Na aliweka agano hilo kwa Mlima Sinai kuwafanya kuwa mali yake ya thamani na taifa takatifu.
  4. Nne, iwapo, kama mkitimiza sehemu yenu ya agano kwa kumtii Mungu, atawapenda na atawabariki zaidi ya watu wengine.
  5. Tano, mkiabudu miungu mingine, hasira ya Mungu itawachoma na itawaondoa katika nchi hii. Bali mtakapotubu na kumtafuta Bwana na kumtii, atawahurumia na kukumbuka ahadi yake.

Baadaye, Musa alipanda Mlima Nebo kuiangalia Kanani. Akafa hapo na kuzikwa na Mungu mwenyewe. Mungu alikuwa amechagua Yoshua kuwa kiongozi wa watu wake. Basi Yoshua aliwaongoza Waisraeli kuvuka Mto wa Yordani na kuanza kuwafukuza Wakaanani na kuchukua Nchi ya Ahadi.