CBS Stories

Swahili Stories

Waamuzi

Yoshua 7-28; Waamuzi; 1 Samweli 1-4

Waisraeli walipokuwa wakishinda Wakanani, makabila kumi na mawili wake walichukua sehemu ya nchi. Ilikuwa kazi yao kuwaondoa Wakanani walioishi hapo ili wasije kuchanganyika nao na kuabudu sanamu zao.

Baada ya kifo cha Yoshua, makabila kumi na mawili walijitawala. Lakini walipojisikia kwamba wamestarehe na kunawiri katika nchi mpya, walisahau alivyowaambia Mungu kufanya. Kila mtu akafanya yaliyokuwa mema machoni pake.

Basi malaika wa Bwana akawaambia watu, “Nilipowatoa Misri nilisema, ‘Msiwaruhusu Wakanani kuishi pamoja nanyi.’ Lakini mmevunja ahadi hii kati yetu. Mmeruhusu Wakanani kuishi nanyi na hamkuvunja madhabahu yao na kuchoma sanamu zao. Kwa hivyo sitawaondoa tena kutoka nchi yenu. Watakuwa miiba ubavuni mwenu na miungu yao itakuwa mitego yenu.”

Na hivyo ndivyo ilifanyika. Kizazi kipya kilimsahau Mungu. Wakaanza kuabudu miungu ya Wakanani na kufanya mambo maovu sana. Maadui wao waliwavamia, na kila wakati Waisraeli walipoenda kupigana, Mungu alikuwa dhidi yao nao walishindwa.

Walipokuwa watumwa tena, walimkumbuka Mungu, kisha wakamlilia awaokoe. Ndipo Mungu aliinua kiongozi aliyewaokoa kutoka kwa maadui. Kila kiongozi aliitwa mwamuzi.

Lakini baada ya muda wangemsahau Mungu tena, na mtindo huu ungeanza tena. Mara kumi na nne katika miaka mia tatu hamsini, Waisraeli waliasi dhidi ya Mungu na kuziabudu sanamu za Wakanani. Kila mara, Mungu aliwaadhibu kama alivyosema alipowapatia Amri Kumi katika Mlima wa Sinai. Lakini kila mara Waisraeli walitubu dhambi zao na wakaanza kutii tena na Mungu aliwasamehe na akawabariki tena na mwamuzi kuwaokoa. Huu unaitwa wakati wa Waamuzi. Gidioni, Debora, na Samsoni walikuwa baathi ya waamuzi. Mwamuzi wa mwisho kuwaokoa wana wa Israeli alikuwa mtu aliyeitwa Samweli. Samweli alipokuwa mvulana, Mungu alizungumza naye, na kumwambia mambo ambayo yangetokea wakati ujao. Alipokuwa akikua, Mungu alikuwa pamoja naye, na yote aliyosema yalitimia. Hivyo watu wote walijua kwamba Samweli alikuwa nabii wa Mungu.