CBS Stories

Swahili Stories

Mwito wa Musa katika Kichaka Kinachowaka

Kutoka 3-4

Musa alikuwa na umri wa miaka arobaini alipokimbia kutoka Misri. Aliishi jangwani kwa miaka arobaini zaidi na akamwoa Sipora, binti Yethro, aliyekuwa kuhani wa Midiani.

Siku moja, Musa alikuwa akichunga kondoo za baba mkwe wake karibu na Mlima Sinai, na malaika wa BWANA akamtokea katika miali ya moto kutoka ndani ya kichaka. Musa akaona kwamba hata ingawa kile kichaka kilikuwa kinawaka moto, hakikuteketea. Kwa hiyo akakaribia kuona maono haya ya ajabu, na Bwana akamwita kutoka ndani ya kile kichaka, "Musa! Musa!"

Musa akajibu, "Mimi hapa."

Mungu akasema, “Usikaribie zaidi. Vua viatu vyako, maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu. Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Nimeona mateso ya watu wangu huko utumwani Misri. Sasa ninapanga kuwaokoa na kuwarudisha katika nchi ya Wakanaani, nchi tele inayotiririka maziwa na asali. Basi sasa nenda, nakutuma kwa Farao ili kuwatoa watu wangu Waisraeli kutoka Misri."

Ndipo Musa akaficha uso wake, kwa sababu aliogopa kumwangalia Mungu. Naye akaanza kubishana na Mungu akisema, "Mimi ni nani hata niende kwa Farao na kuwatoa Waisraeli kutoka Misri? Je, Waisraeli wasiponiamini? Na je, wakiuliza ni nani aliyenituma? Jina lake ni nani?"

Mungu akasema, "MIMI NIKO AMBAYE NIKO. Hivi ndivyo utakavyowaambia Waisraeli: ‘ MIMI NIKO amenituma kwenu.’” Pia Mungu akamwambi Musa, “Nitakuwa pamoja nanyi. Na hii itakuwa ishara kwako kwamba Ndimi Mimi niliyekutuma: Utakapowatoa watu kutoka Misri, mtaniabudu kwenye mlima huu.”

Mungu akampa Musa ishara nyingine mbili ili kuwaonyesha watu ili waweze kuamini kile alichokisema. Akasema, "Itupe chini fimbo yako." Musa alifanya

hivyo, na ikawa nyoka! Ndipo Mungu akasema, “Sasa mshike kwa mkia.” Musa alipoiokota, ikawa fimbo tena. Kisha Mungu akamwambia aweke mkono wake ndani ya vazi lake. Alipoutoa, ulikuwa umefunikwa na ukoma, lakini alipourudisha tena

ukapona. Kisha Mungu akasema, “Utawaonyesha Waisraeli ishara hizi ili wapate kuamini kwamba Bwana, Mungu wa baba zao, amekutokea."

Mungu pia aliahidi kumtuma Haruni ndugu ya Musa pamoja naye. Kwa hiyo Musa akakubali na kurudi Misri.