Amri na Ahadi
Baada ya Mungu kuchanganya lugha kwenye mnara wa Babeli kulikuwa na mtu mmoja aliyeitwa Abramu. Alikuwa na umri wa miaka sabini na mitano. Mke wake, Sarai, alikuwa mkongwe pia, nao hawakuwa na watoto. Siku moja, Mungu alimtokea Abramu na akamwambia, “Abramu, ondoka katika nchi yako, waache watu wako na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha. Mimi nitakufanya taifa kubwa, nitafanya jina lako kuu, nitabariki watakaokubariki, na nitalaani watakaokulaani na kupitia kwako mataifa yote duniani yatabarikiwa.”
Kanaani na Misri
Abramu akamchukua Sarai mkewe pamoja na Lutu mwana wa ndugu yake nao wakasafiri mpaka nchi ya Kanani. Walipofika hapo Mungu akamwambia “Hapa ndipo mahali. Nitawapa uzao wako nchi hii.” Wakati huo kulikuwa na njaa kuu katika nchi, naye Abramu akashuka kwenda nchi ya Misri pamoja na familia yake. Huko Misri, Abramu aliwaogopa Wamisri akawadanganya kuhusu mke wake badala ya kumwamini Mungu kumlinda. Lakini hata ingawa alifanya hiyo dhambi, Mungu aliwalinda Abramu na mkewe. Pia alimbariki na mali nyingi sana wakati huo.
Ugomvi na Lutu
Abramu na familia yake waliporudi Kanani kutoka Misri, walikuwa na wanyama wengi. Wote wawili, Abramu na Lutu walikuwa matajiri, lakini nchi haikuwatosha kukaa pamoja kwa ajili ya wanyama wao. Ukazuka ugomvi kati ya wachunga mifugo wa Abramu na wale wa Lutu. Abramu akamwambia Lutu, “Tusigombane, sisi ni jamaa moja. Ebu angalia nchi yote. Kama ukielekea kushoto nitakwenda kulia, kama ukielekea kulia, mimi nitakwenda kushoto.” Lutu akatazama akaona lile bonde lote akaona linapendeza, lilikuwa na maji tele na nyasi, chakula cha wanyama. Akamwacha Abramu aliyeishi kwenye milima iliyojaa mawe. Lutu alihama akaishi Sodoma, mji uliokuwa na watu waovu.
Kumwamini Mungu
Baada ya muda, Bwana alimtokea Abramu na akamwambia, “Usiogope, nimekupa nchi hii yote, mimi ni ngao yako na thawabu yako kubwa sana.” Lakini Abramu akasema, “Itakuwa faida gani ukinipa nchi hii yote kama sina hata mtoto atakayekuwa mrithi wangu?”
Naye Mungu akamwambia Abramu, “Utakuwa na mwana kutoka katika mwili wako mwenyewe.” Akamleta nje, akasema, “Tazama mbinguni, na uzihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu.” Kisha akamwambia, “Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.” Naye Abramu akamwamini BWANA, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki.
Mungu akamwongoza Abramu kutoa dhabihu maalum ambapo Mungu alimtokea akiwa katika usingizi mzito. Akamwambia Abramu wazao wake watakuwa watumwa na watateswa kwa miaka mia nne kwenye nchi ya kigeni lakini Mungu atawaokoa kutoka taifa hilo. Baadaye Mungu alibadilisha jina lake liwe Abrahamu na jina la mkewe liwe Sarah.