CBS Stories

Swahili Stories

Mwanamke Msamaria

Yohana 4:1-45

Baada ya pasaka Yesu na wanafunzi wake walirudi Galilaya. Mara hii walitumia njia fupi ambayo ilienda moja kwa moja kaskazini kutoka Yerusalemu kupitia nchi ya vilima iliyoitwa Samaria.  Wayahudi waliwachukia Wasamaria. Wasamaria walitokana na wana wa Waisraeli walipooana na Waashuri wakati Ashuri ilipovamia na kushinda ufalme wa kaskazini miaka 750 iliyotangulia. Kwa hivyo Wasamaria walikuwa watu wachafu wasiokuwa na tumaini na mtu yeyote ambaye alihusiana nao alikuwa akihesabiwa mchafu pi.

Walipokuwa katika nchi ya Samaria, Yesu na wanafunzi wake walifika kwenye kisima ambacho babu yao, Yakobo alikuwa amechimba. Ilikuwa karibu na adhuhuri naye Yesu alikuwa amechoka. Kwa hivyo aliketi kwenye kisima wakati wanafunzi wake walipoenda mjini kununua chakula.

Halafu mwanamke Msamaria fulani alikuja kuteka maji, Yesu alimwambia, “Nipe maji ninywe.”

Alistaajabu, Wewe ni mwanamume Myahudi nami ni mwanamke Msamaria. Je, umawezaje kuniuliza nikupe maji?” (Kwa maana Wayahudi hawakuchangamana na Wasamaria.)

Yesu akasema, “Ungalijua karama ya Mungu naye akuulizaye umpe maji, ungemwuliza naye angekupa maji ya uzima.”

Akajibu, “Bwana, huna kitu cha kutekea na kisima ni kirefu. Utapata wapi haya maji ya uzima?”

Yesu akamwelezea, “Mtu anapokunywa maji kutoka kwa kisima hiki, yeye hupata kiu tena. Lakini yeyote anayekunywa maji ninayompa, hataona kiu tena. Maji nitakayompa yatakuwa chemichemi ya maji yakibubujika uzima wa milele kwake.”

“Bwana, nipe maji haya ili nisione kiu tena na kuja hapa katika kisima hiki kuteka maji.”

Yesu akamwambia, “Nenda umwite mumeo, na uje hapa.”

“Sina mume,” mwanamke huyo alimjibu.

“Hapo umesema ukweli.” Yesu akasema. “Umekuwa na waume watano na hata yule unayeishi naye si mumeo.”

“Bwana, naona kwamba wewe u nabii.  Babu zetu waliabudu katika mlima huu lakini ninyi Wayahudi mnasema kwamba Yerusalemu ndipo pahali ambapo watu wanapaswa kuabudu.”

Yesu akamwambia, “Wakati unakuja ambao hamtaabudu hapa au pale. Saa yaja, nayo ipo, ambapo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika Roho na ukweli, kwa maana Baba anawatafuta watu kama hao wamwabudu, Nao wamwabuduo lazima wamwabudu katika roho na ukweli.”

“Naam, najua kwamba Masihi anakuja,” mwanamke huyo akamwambia, “Na atakapokuja, atatuelezea kila kitu.”

Kisha Yesu akamwambia kwa wazi, “Mimi ndiye.”

Mwanamke huyo akauacha mtungi wake kisimani akarudi mjini na kuambia kila mtu. Njooni mwone yule aliyeniambia kila kitu ambacho nimefanya. Je, aweza kuwa ndiye Masihi?” Kwa hivyo walirudi kisimani naye kumwona Yesu.

Wengi wao wakamwamini Yesu kwa sababu ya yale mwanamke huyo aliyoshuhudia, nao wakamsihi asiondoke kwa hivyo Yesu alikaa siku mbili zaidi, akiwafunza watu, na hata wengi zaidi wakamwamini.

Kisha wakamwambia huyo mwanamke, “Sasa tunaamini wala si kwa sababu ya yale uliyotuambia, lakini tumesikia sisi wenyewe na tumejua kwamba mtu huyu kwa kweli ndiye Mwokozi wa ulimwengu.”