CBS Stories

Swahili Stories

Mfalme Daudi

1 & 2 Samweli, Hasa 1 Samweli 16, 17 na 2 Samweli 6, 7, 11, 12

Baada ya Mungu kumkataa Sauli kama mfalme, alimwongoza Samweli kumtembelea mtu aliyeitwa Yese katika mji wa Bethlehemu, ili kutafuta mfalme aliyechaguliwa. Samweli alifikiri Mungu angemchagua mmoja wa wana wakubwa wa Yese, lakini Mungu alisema, “Hapana. Mwanadamu anaangalia nje ya mtu lakini Mungu anaangalia moyo.” Kwa hivyo alimchagua mwana mdogo zaidi aliyeitwa Daudi. Samweli akamtia mafuta. Na Roho wa Mungu akawa naye tangu siku hiyo.

Mfano mmoja wa usaidizi wa Roho wa Mungu kwa Daudi, ulifanyika wakati Daudi bado alipokuwa mvulana. Alienda kuwatembelea ndugu zake katika jeshi la Israeli lilipopigana na jeshi la Wafilisti. Daudi alipofika kambi ya jeshi aliona kwamba Goliathi alikuwa akiwadhihaki Waisraeli na Mungu wao, kwa sababu wote waliogopa kupigana naye. Daudi aliona kile kinafanyika na akakasirika akasema atapigana naye. Hata ingawa alikuwa mtu mdogo ambaye hakujua kutumia silaha za vita, Daudi alijua kwamba Mungu atamsaidia kama alivyomsaidia alipokuwa mchungaji alipowalinda kondoo wake kutokana na wanyama kama simba. Basi Daudi alipopambana na Goliathi, alimwua na kombeo na jiwe na akawapatia Waisraeli ushindi.

Sauli aliendelea kuwa mfalme kwa miaka mingine kumi na mitano. Alimweka Daudi kuwa msimamizi wa baadhi ya askari wake, lakini Sauli angeskia wanawake wakiimba, “Sauli ameua maelfu, lakini Daudi ameua makumi ya maelfu!” Kwa sababu ya wivu wake, mara nyingi sana Sauli alikuwa akijaribu kumwua Daudi. Bali Daudi kamwe hakujaribu kumwumiza Sauli, naye Mungu alimlinda Daudi. Baada ya Sauli na wanawe kufa katika vita, viongozi wa watu walimtia Daudi mafuta ili awe Mfalme wa Israeli kama Samweli alivyofanya miaka mingi iliyopita. Daudi alikuwa na miaka thelathini alipokuwa Mfalme na akatawala kwa miaka arobaini.

Daudi alikuwa mpiganaji mkuu, naye alimtumaini Mungu sana. Ila, alifanya dhambi nyingine kubwa sana katika maisha yake, lakini alitubu na akasamehewa na Mungu. Daudi alipokuwa amewashinda adui zake wote, alileta sanduku la agano katika Yerusalemu, mji mkuu wake. Daudi alitaka kujenga nyumba kuu, hekalu, kwa Mungu.

Lakini Mungu, akatuma ujumbe kwake kupitia kwa nabii Nathani akasema, “Hutajenga nyumba yangu kwa sababu umemwaga damu nyingi, lakini kijana wako ataijenga.

Ninakuahidi kwamba utakuwa na mwana kukaa katika kiti chako cha enzi milele na ufalme wako utakaa milele.” Naye Daudi alimsifu Mungu kwa ajili ya ahadi zake.

Hata ingawa Daudi alikuwa mwenye dhambi aliyehitaji neema ya Mungu, alikuwa mtu aliyependeza moyo wa Bwana. Mungu alimtumia kuziandika nyimbo nyingi za kumwabudu katika neno lake.