CBS Stories

Swahili Stories

Mapigo Tisa

Kutoka 7-11

Baada ya Musa na ndugu yake Haruni kukutana na wazee wa Israeli, walimwendea Farao wakasema, “Mungu wa Israeli asema, “Uruhusu watu wangu kuenda, ili wapate kuniabudu jangwani.”

Farao akasema, “Bwana ni nani, hata niisikize sauti yake? Mimi simjui Bwana wala sitawapa Waisraeli ruhusa waende zao. Kwa nini mnawachukua watu kutoka kazi yao? Nendeni sasa!” Farao alikasirika kwa hivyo alisababisha kazi ya Waisraeli iwe ngumu zaidi. Waisraeli wakamlilia Musa.

Musa akamwomba Mungu na Mungu akasema, “Nenda waambie Waisraeli, ‘Nimekisikia kilio chenu na nitawaokoa kutoka kwa Misri na nitawafanya watu wangu na nitawaleta katika nchi ambayo nimewaahidi Abrahamu, Isaka, na Yakobo.”

Basi Musa na Haruni walimrudia Farao na mashindano kati ya mfalme wa Misri na Mungu wa Israeli yakaanza. Kwanza, Haruni alimwonyesha ishara ya fimbo iliyobadilika na kuwa nyoka. Lakini Farao hakuamini akakataa kuwaruhusu Waisraeli kuenda. Kisha mapigo yakaanza. Musa alinyoosha mkono wake juu ya maji ya Misri na mito na maziwa na maji yote yalibadilika kuwa damu hata maji yaliokuwemo ndani ya mitungi. Samaki wote katika Mto wa Nile walikufa na mto ulinuka vibaya na watu, hawakuweza kunywa maji yake. Hata hivyo, Mungu akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu na akakataa kuwaruhusu waende.

Kwa hivyo, Mungu alilituma pigo la vyura kwa nchi yote na Farao akamwita Musa, “Mwombe Bwana kuwaondoa vyura hawa na nitawaruhusu waende.” Musa akafanya hivyo lakini Farao akabadilisha mawazo yake.

Kisha Haruni alinyoosha fimbo yake na kupiga mavumbi yote ya Misri yakabadilika kuwa pigo la chawa. Waganga hawakuweza kuiga pigo hilo kama walivyofanya kwa mapigo mengine na wakasema, “Hiki ndicho kidole cha Mungu!” Lakini Farao akakataa tena kusikiliza.

Basi Mungu aliyatuma mapigo mengine sita kwa Wamisri ila hayakuwaguza Waisraeli hata kidogo. (Yalikuwa mapigo kama mainzi, magonjwa ya mifugo, majipu, mvua ya mawe, nzige, na giza nzito.) Kila pigo lilipokuja, Farao alisema “Ndiyo, waende.” Lakini baada ya pigo kuondolewa alikuwa akikataa waende.

Kwa hivyo Mungu akamwambia Musa, “Nimefanya moyo wa Farao kuwa mgumu ili kuwaadhibu Wamisri kwa miungu yao. Ninafanya ishara hizi ili mtawaambia watoto wenu na wajukuu wenu hata mjue kwamba mimi ndimi Bwana! Nitalileta pigo lingine moja kwa Misri, halafu Farao atawafukuza kabisa.”