CBS Stories

Swahili Stories

Kushikwa na Hukumu ya Yesu

Matthayo 26:36-50; Yohanna 18:12-19:16

Baada ya Yesu na wanafunzi wake kumaliza kula Pasaka, aliwaleta nje ya mji kwenye Mlima wa Mizeutuni katika bustani iitwayo Gethsemane. Akawaambia “Kesheni mkiomba ili msiingie majaribuni.” Akachukua Petro, Yakobo, na Yohana akaenda nao hatua chache, akasema, “Roho yangu ina huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.” Akaenda mbele kidogo akaanguka na kuomba akisema, “Baba yangu ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke, lakini si kwa mapenzi yangu ila tu vile utakavyo wewe.”

Yesu alipomaliza kuomba vile akarudi kwa wanafunzi wake akawakuta wamelala akawaamsha na kuwaambia, “Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?” Na wakaona haya sana. Akaenda tena mara ya pili kuomba akisema, “Baba yangu niepushe kikombe, lakini si kulingana na mapenzi yangu bali mapenzi yako yatimizwe.” Akaja tena mara ya pili akakuta wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito.  Kisha akarudi kuomba mara ya tatu na akaja akawaambia wanafunzi wake, “Amkeni! Saa imekaribia na yule msaliti yu karibu.”

Alipokuwa katika kusema, Yudas akaja na kundi kubwa la jeshi akamsalimu Yesu kwa busu na askari wakamshika Yesu wakaenda naye na wanafunzi wote wa Yesu wakatoroka kwa uoga.

Kwanza maaskari na viongozi wa Wayahudi walimpeleka Yesu kwa nyumba ya Kuhani Mkuu. Mashahidi walimnenea mambo mengi ya uwongo lakini alikuwa kimya. Kuhani Mkuu akamwuuliza Yesu. “Hujibu neno, mwanaume? Kwa nini husemi kitu kujitetea? Tuambie, wewe ndiwe Kristo Mwana wa Mungu?” Yesu akajibu, “Ndio mimi ndimi.” Kuhani Mkuu aliposikia hayo, akararua mavazi yake akisema “Amekufuru! Tuna haja gani tena na mashahidi?” Na watu wote wakasema, “Ana hatia na inampasa afe.”

Kulipokuwa asubuhi, viongozi wa Wayahudi walikuwa wamemaliza kuuliza Yesu maswali, wakamchukua wakamleta mbele ya Pilato, aliyekuwa kiongozi wa Kirumi katika pahali hapo. Pilato akawauliza, “Ni kosa gani mtu huyu amefanya? Viongozi wa Wayahudi wakasema, “Yeye anasema ni mfalme.” Pilato akamwuuliza Yesu, “Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?” Yesu akasema, “Ndiyo, lakini ufalme wangu si wa ulimwengu huu.” 

Ndipo Pilato akamtwaa Yesu kwa askari wakampiga mijeledi. Baada ya kumpiga Yesu sana, Pilato akarudi kuongea na Wayahudi akisema, “Mtu huyu namleta kwenu tena, mpate kujua ya kuwa mimi sioni hatia yoyote kwake.”

Wakapiga kelele wakisema, “Hapana! Msulubishe, msulubishe!” Pilato akawaambia, “Mimi sioni hatia kwake.” Basi Wayahudi wakapaza sauti wakisema, “Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari katika Rumi!” Hatimaye Pilato aliwapa Yesu mikononi mwao ili asulubishwe.

Huu ndio mwisho wa hadithi.