Hii ni hadithi ya Yesu jinsi alimponya mtu aliyepooza.
Baada ya Yohana kumbatiza Yesu, Yesu alizunguka mji baada ya mwingine akihubiri. Na popote Yesu alipoenda, umati mkubwa ulimfuata. Na hivi ndivyo ilikuwa ikifanyika kila wakati.
Siku moja Yesu alikuja Kapernaumu na akaingia katika nyumba moja. Aliketi na kuanza kufunza, na umati ulijaza nyumba na hata nje ya nyumba. Watu walikuwa wakiangalia kwenye madirisha na milango. Kila mtu alimsikiliza Yesu akifunza.
Sasa kulikuwa na mtu aliyepooza huko Kapernaumu. Alikuwa na marafiki wane. Hawa walimpeleka kwa Yesu, lakini hawakuweza kumfikia Yesu kwa maana watu walikuwa wengi sana. Walijaribu njia yoyote bila kufaulu. Mwishowe, walipanda ngazi kando ya nyumba hadi kwenye paa. Halafu walitomboa shimo kwenye paa. Wakafunga godoro la mgonjwa kwa kamba, na wakamshusha mtu huyo mbele ya Yesu. Yesu alipoona imani yao alimwambia mtu aliyepooza, “Dhambi zako zimesamehewa.”
Papo palikuwa na walimu wa sheria wakimsikiliza Yesu. Waliposikia maneno haya walikasirika sana na Yesu. Waliwaza mioyoni mwao, “Anawezaje kusema hivyo! Ni Mungu tu anaweza kusamehe dhambi!”
Lakini Yesu alijua kile walivyofikiri akawaambia, “Ni lipi gumu - mimi kusema, ‘Dhambi zako zimesamehewa’ au kusema, ‘Inua! Chukua kitanda chako! Uende?’ Sasa nataka mjue kwamba Mwana wa Adamu ana mamlaka duniani kuzisamehe dhambi.” Kisha Yesu akamwambia mtu aliyepooza, “Ondoka ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako.”
Naye akafanya hivyo! Mara akaondoka akajitwika godoro lake akatoka mbele yao wote. Wakastaajabu wakamtukuza Mungu wakisema, “Namna hii hatujapata kuiona kamwe!”
Huu ndio mwisho wa hadithi.