Mke kwa Isaka
Abrahamu alipokuwa na miaka mia moja na thelithini na saba, mkewe aliaga dunia na Abrahamu akamzika huko Hebroni. Wakati huo, Isaka alikuwa na miaka karibu arobaini na hakuwa ameoa. Kwa hivyo Abrahamu akamtuma mtumishi wake kaskazini Siria kwenda kwa watu wa ukoo wake alikotoka Abrahamu ili kumtafutia Isaka mke kwa sababu Abrahamu hakutaka Isaka kumwoa binti wa Kikanaani.
Mtumishi alipofika huko Siria, alimwomba Mungu kumwonyesha msichana anayefaa. Naye Mungu akamwongoza kwa Rebekah. Rebekah alikuwa binti wa mpwa wa Abrahamu aliyekaa huko Siria. Rebekah na babake walikubali ndoa. Basi Rebeka alienda Kanaani pamoja na mtumishi wa Abrahamu, na akaolewa na Isaka. Baada ya haya yote, Abrahamu aliaga dunia na Isaka akamzika Hebroni alipozikwa Sara.
Kuzaliwa kwa Isaka na Wavulana wa Rebeka
Kwa muda mrefu, Rebeka hakuweza kupata mimba. Kwa hivyo Isaka alimwombea Rebekah. Mwishowe baada ya miaka ishirini, alijifungua mapacha wavulana. Rebeka alipokuwa mjamzito, watoto walishindana tumboni mwake. Mungu akamwambia, “Mataifa mawili yako tumboni mwako. Mkubwa atamtumikia mdogo.” Walimwita mzaliwa wa kwanza Esau. Baada ya Esau kuzaliwa, ndugu yake alitoka na mkono wake unamshika Esau kisigino. Kwa hivyo akaitwa Yakobo, maana yake “mdanganyifu.”
Kudharau Haki ya Kuzaliwa
Kwa sababu ya kuwa mzaliwa wa kwanza, Esau angepata haki ya uzao wa kwanza, (yaani urithi mara mbili), na baraka ya ahadi ya Mungu kuwabariki uzao wa Abrahamu kupitia kwake. Walipokuwa wakikua, Esau akawa mwindaji aliyependa kuwa mwituni.
Isaka alimpenda Esau zaidi kwa maana alipenda nyama alizomletea. Lakini Yakobo alikuwa mtulivu aliyekaa hemani. Na alipendelewa sana na mamake.
Siku moja Yakobo alipokuwa akipika mchuzi, Esau alirudi nyumbani kutoka msituni akiwa na njaa kubwa. Akamwambia Yakobo, “Nipe chakula nile.” Yakobo akakataa akasema, “Sitakupatia mchuzi usiponiuzia haki ya urithi wako.”
Esau akamjibu, “Niko karibu kufa kwa njaa. Haki hii ina faida gani kwa mtu aliyekufa?” Akamwapia kumwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa bakuli moja ya mchuzi. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
Kuiba Baraka
Muda ulipita na Isaka alimwita Esau akasema, “Mimi nimekuwa mkongwe. Sijui nitaishi muda gani zaidi. Nenda uwinde nyama, na uipike jinsi nipendavyo. Ningependa kukupatia baraka yangu kabla nife.”
Lakini Rebeka alikuwa akisikiliza, na Esau alipokuwa akiwinda, Rebeka alimsaidia Yakobo kumdanganya baba yake aliyekuwa kipofu akifikiria huyu Yakobo alikuwa Esau akija na nyama nzuri. Kwa hivyo Isaka alimbariki Yakobo na baraka ya Esau aliyekuwa
mzaliwa wa kwanza. Esau alipotambua kuwa Yakobo alimwibia baraka zote mbili, yaani urithi na baraka ya mzaliwa wa kwanza, alighadhabika na akaapa kumwua nduguye.
Hivyo Rebekah akamwambia Yakobo, “Nisikilize! Ni bora zaidi ukienda kukaa na ndugu yangu Labani huko Siria mpaka Esau atakapopoa. Nitakwambia utakoweza kurudi salama.”
Pia Rebeka akamwambia Isaka, “Nimechoka na wake wa kigeni wa Esau. Kama Yakobo atamwoa mmoja wao, sina haja ya kuishi.”
Kwa hivyo Isaka akamwambia Yakobo, “Usimwoe msichana Mkanaani. Badala yake, sasa nenda Siria kumchukua binti moja wa mjomba wako Labani.” Kwa hivyo Yakobo akaenda Siria.