(*Ilani - Kwa wakati huu Mungu alikuwa amebadilisha majina ya Abramu na Sarai kuwa Abrahamu na Sara.)
Hatimaye, baada ya miaka ishirini na mitano Mungu kumwahidi Abrahamu kumfanya taifa kuu, Sara, katika ukongwe wake, alijifungua mtoto wa kiume kama vile Mungu alikuwa amemwahidi. Wakamuita jina lake Isaka, maanake ‘kucheka’ kwa sababu Sara alicheka wakati Mungu alipomwambia, atajifungua mtoto. Basi Isaka alikua na akawa kijana.
Baada ya miaka kadhaa, siku moja Mungu alimtokea Abrahamu akamwambia, “Abrahamu, umchukuwe mwanao Isaka, mwana wako wa pekee umpendaye, uende katika nchi ya Moria. Mtoe huko kama sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima.” Siku iliyofuata asubuhi, Abrahamu alikusanya kuni na kuziweka juu ya punda, kisha akawaita watumishi wawili. Abrahamu akabeba kisu na moto wakaenda na Isaka kuelekea mahali Mungu alikuwa amemwambia.
Abrahamu alipoona mlima Moria kwa umbali, akawaeleza watumishi wake, “Kaeni hapa pamoja na punda. Mimi na kijana tutaenda mlimani kuabudu, kisha tutarudi. Abrahamu akachukua kuni akamtwika Isaka, yeye mwenyewe akachukua moto na kisu. Walipokuwa wakienda pamoja, Isaka akamwuliza Abrahamu, “Moto na kuni zipo. Je, mwanakondoo wa sadaka yuko wapi?” Abrahamu akamjibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atajipatia mwanakondoo kwa ajili ya hiyo sadaka.”
Walipofika mlima Moria, Abrahamu akajenga madhabahu, kisha akaweka kuni juu yake. Akamfunga Isaka mwanawe na akamlaza kwenye madhabahu. Kisha akachukua kisu ili amchinje mwanawe, punde malaika wa Bwana akasema, “Abrahamu! Usimdhuru mwanao! Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu kwa sababu, haukunizuia mwanao, mwanao wa pekee."
Abrahamu alipogeuka, akaona kondoo wa kiume amenaswa kwa pembe zake katika kichaka. Abrahamu akamtoa Isaka kwenye madhabahu na kumweka yule kondoo badala yake. Abrahamu akapaita mahala pale, “Yehova-yire." Maanake, "Katika mlima wa Bwana, itapatikana."
Baada ya Abrahamu kumtoa kondoo kama dhabihu, malaika wa Bwana akamwambia, “Nitakubariki na kuzidisha uzao wako kama nyota za angani.
Kupitia uzao wako mataifa yote duniani yatabarikiwa.”