Wakati huu wa kanisa la kwanza la Yerusalemu, waamini wanaozungumza Kigiriki walilalamika dhidi ya waumini wa Kiebrania kwa sababu wajane wao walikuwa wakipuuzwa katika ugawaji wa chakula wa kila siku. Mitume wakakusanyika pamoja na wanafunzi wengi, wakasema, "Si sawa sisi kuacha kulihubiri neno la Mungu na kuhudumia mezani." Kisha wakawaagiza wanafunzi wachague wanaume saba waliokuwa na sifa nzuri na waliojaa Roho na hekima ili wawekwe rasmi na kutekeleza wajibu huu ili waweze kujitoa wenyewe kwa maombi na kwa huduma ya neno.
Kisha mitume wakaweka mikono yao juu ya wale saba waliochaguliwa na kuwaombea. Stefano alikuwa mmoja wa watu hawa. Na Neno la Mungu likaendelea kuenea kwa kasi.
Baada ya muda, viongozi wa dini walimkasirikia Stefano kwa sababu ya baadhi ya maajabu na ishara alizokuwa akizifanya. Waliunda mashahidi wa uwongo wakimshtaki kwa kufundisha dhidi ya sheria ya Musa na dhidi ya Hekalu. Stefano aliletwa mbele ya Kuhani Mkuu na Baraza, akamwuliza Stefano,
“Je, mashtaka haya ni ya kweli?
Stefano alijibu kwa kuwakumbusha juu ya uaminifu wa Mungu kwa Waisraeli waasi mara nyingi na kwa ahadi zake katika Agano la Kale.
Alipitia hadithi za Ibrahimu, Yosefu, Musa, Yoshua, Daudi, Sulemani, hata manabii na uhamisho wa Babeli, akionyesha jinsi Agano lote la Kale lilivyokuwa likimlenga Kristo.
Stefano akasema, “Enyi wenye shingo ngumu! Mioyo yenu na masikio yenu bado hayajatahiriwa. Ninyi mmefanana na wazee wenu: Siku zote mnampinga Roho Mtakatifu!