Wakati kanisa lilipokuwa likienea katikati ya mateso, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Simoni, ambaye hapo awali alikuwa akifanya uchawi katika mji wa Samaria na kuwashangaza watu, akijisifu kwamba yeye mwenyewe ni mtu mkuu. Watu walimwamini na kudhani ana nguvu za Mungu kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa akiwashangaza kwa uchawi wake. Lakini walipomwamini Filipo akihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. Hata Simoni mwenyewe aliamini, na baada ya kubatizwa akaendelea na Filipo. Alipoziona ishara na miujiza mikubwa ikifanyika, alistaajabu.
Mitume kule Yerusalemu waliposikia kwamba Samaria imelipokea neno la Mungu, waliwatuma kwao Petro na Yohana. Walishuka na kuwaombea ili wampokee Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu alikuwa bado hajashuka juu ya yeyote kati yao, lakini walikuwa wamebatizwa tu katika jina la Bwana Yesu. Kisha wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu. Basi Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho kwa kuwekewa mikono ya mitume, akawatolea fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemwekea mikono yangu apokee Roho Mtakatifu.
Lakini Petro akamwambia, "Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa ulidhani kwamba ungepata karama ya Mungu kwa fedha! Huna sehemu katika huduma hii kwa sababu moyo wako si sawa mbele za Mungu. Tubu, basi, uache uovu wako huu, umwombe Bwana; labda atakusamehe kwa kuwa na mawazo hayo moyoni mwako; maana naona umejaa uchungu na mateka wa dhambi."
Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, lisinipate neno lo lote katika hayo mliyosema.
Walipokwisha kushuhudia na kuhubiri neno la Bwana, Petro na Yohana walirudi Yerusalemu, wakihubiri Injili katika vijiji vingi vya Wasamaria.