Book of Acts

Swahili Stories

Petro na Yohana Mbele ya Viongozi wa Dini

Matendo 4:1-14

Baada ya yule kiwete kuponywa, makuhani, walinzi wa hekalu, na Masadukayo walikuja kwa Petro na Yohana. Walifadhaika sana kwa sababu mitume walikuwa wakiwafundisha watu, wakitangaza katika Yesu ufufuo wa wafu. Basi wakawakamata Petro na Yohana na kuwaweka jela hadi kesho yake. Lakini wengi waliosikia ule ujumbe waliamini; kwa hiyo hesabu ya wanaume walioamini ikaongezeka kufikia kama elfu tano.

Kesho yake kuhani mkuu na watawala wengine wakakutana na kuwaleta Petro na Yohana mbele yao na kuanza kuwauliza: “Mlifanya jambo hili kwa nguvu gani au kwa jina gani?”

Ndipo Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akawaambia, Ikiwa mnauliza juu ya tendo hili la wema alilofanyiwa mtu kiwete, ni kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulubisha lakini ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, ndipo mtu huyu anasimama mbele yenu akiwa mzima. Kwa maana Yesu ndiye 'jiwe mlilokataa ninyi waashi, ambalo limekuwa jiwe kuu la msingi.' Wokovu haupatikani kwa mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”

Basi, walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwafahamu ya kuwa hawakuwa na elimu, watu wa kawaida, walishangaa. Nao wakatambua kwamba walikuwa pamoja na Yesu. Lakini walipomwona yule mtu aliyeponywa amesimama karibu nao, hawakuwa na la kusema kwa kumpinga.

Kwa hiyo wakawaonya vikali wasiseme wala kufundisha tena kwa jina la Yesu. Petro na Yohana wakajibu, “Ni lipi lililo sawa machoni pa Mungu, kuwasikiliza ninyi au Mungu? Ni lazima sisi tunene kuhusu yale tuliyoyaona na kuyasikia. [tuliyoyashuhudia]