Wakati wa kifo cha Stefano, kijana mmoja anayeitwa Sauli alikuwapo na alikubali kuuawa kwake. Siku hiyo kukatokea mateso makubwa dhidi ya kanisa la Yerusalemu, na wote wakatawanyika katika sehemu za Yudea na Samaria isipokuwa mitume. Watu waliomcha Mungu walimzika Stefano na kuomboleza sana kwa ajili yake. Lakini Sauli alianza kuliharibu kanisa, akiingia nyumba kwa nyumba, akawaburuta wanaume kwa wanawake na kuwatia gerezani. Basi wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakihubiri neno.
Filipo, mmoja wa wale mashemasi saba waliowekwa awali, alishuka mpaka Samaria na kuwahubiria Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno ya Filipo, waliposikia na kuona ishara alizozifanya.
Kwa maana pepo wachafu waliwatoka watu wengi waliokuwa nao wakilia kwa sauti kuu, na wengi waliopooza na vilema wakaponywa. Basi kukawa na furaha nyingi katika mji ule.