Siku ya Pentekoste ilipofika, wanafunzi walikuwa wamekusanyika wote mahali pamoja. Ghafla, sauti kama ya upepo mkali ikavuma kutoka mbinguni, ikajaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Na zikawatokea ndimi zilizogawanyika kama moto na zikakaa juu ya kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine kama Roho alivyowajalia kutamka.
Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu kutoka katika kila taifa chini ya mbingu. Kwa sauti hii umati wa watu ukakusanyika, wakashangaa, kwa sababu kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa na kustaajabu wakisema, “Je, hawa wote wanaosema si Wagalilaya?
Wote wakashangaa na kufadhaika wakiambiana, Maana yake nini hii?
Lakini wengine wakadhihaki, wakisema, Wamenywa divai mpya.
Basi, Petro akasimama, akauambia umati wa watu waliokusanyika huko Yerusalemu, akisema, Hawakulewa, ni saa tatu ya asubuhi. Kisha akaeleza kwamba kumimiwa huku kwa kimiujiza kwa Roho Mtakatifu kulikuwa utimilifu wa unabii wa Yoeli alipotangaza kwamba katika siku za mwisho Mungu angemimina Roho wake juu ya watu wote. Ungekuwa wakati ambapo “kila mtu atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.” Petro akawaambia, "Mungu amemfanya Yesu, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Masihi." Pia aliwaambia kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Na kwamba walikuwa wote ni mashahidi.
Makutano waliposikia hayo wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, tufanye nini, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu, kwa maana ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita kwake.
Basi wale waliolipokea neno lake wakabatizwa, watu wapatao 3,000 siku hiyo.