CBS Stories

Swahili Stories

Yesu Akawaita Wanafunzi Wake

Luka 5:1-11, 27-31; 6:12-15

Siku moja Yesu alikuwa amesimama kando ya ziwa Galilaya na makutano ya watu walimsongea walisikilize neno la Mungu. Akaona vyombo viwili kando ya ziwa. Akaingia ndani ya chombo kimoja chake Simoni, akamwuliza akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi akawafunza watu akiwa chomboni.

Hata alipomaliza kunena, akamwambia Simoni, “peleka chombo chenu kilindini mkashushe nyavu zenu mvue samaki.” Simoni akamjibu akamwambia, “Bwana mkubwa tumefanya kazi usiku kucha tusipate kitu, lakini kwa neno lako nitashusha nyavu.” Basi walivyofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika wakawapungia mikono wahirika wao waliokuwa katika chombo kingine waje kuwasaidia, wakaja wakajaza vyombo vyote viwili hata vikataka kuzama.

Simoni Petro alipoyaona haya alianguka magotini mwa Yesu akisema, “Ondoka kwangu kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi.” Kwa maana alishikwa na mshangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, Yakobo na Yohana wana wa Zebedayo kwa sababu ya wingi wa samaki waliowapata. Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope kuanzia sasa utakuwa ukivua watu.  Wakaviegesha vyombo vyao vuoni wakaviacha na wakamfuata Yesu.

Baada ya hayo akatoka akaona mtoza ushuru jina lake Lawi (Matayo) akiwa ameketi forodhani akamwambia, “nifuate.” Lawi akaamka akaacha vyote akaondoka akmfuata. Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani kwake. Palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengine katika karamu. Lakini Wafarisayo na waandishi wao wakawanungunikia wanafunzi wake wakisema, “kwa nini (mbona) mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi. Yesu akawajibu akawaambia, “Wenye afya hawana haja na tabibu (daktari). Isipokuwa ni wale tu wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki bali wenye dhambi wapate kutubu.”

Ikawa tena siku moja Yesu alienda mlimani kuomba akakesha usiku kucha akimwomba Mungu na asubuhi yake aliwaita wanafunzi wake akawachagua kumi na wawili miongoni mwao ambao aliwaita mitume. Simoni (aliyemwita Petro) na Andrea, nduguye, na Yakobo na Yonana, Matayo na wengineo pamoja na Yudas Iskarioti ambaye mwishowe alimsaliti.