CBS Stories

Swahili Stories

Yakobo, Laban, na Familia ya Yakobo

Mwanzo 29:15-35

Baada ya ndoto yake kuhusu ngazi, Yakobo akaenda zake mpaka nchi ya mjomba wake Labani. Baada ya Yakobo kukaa kwa Labani mwezi mzima, Labani akamwambia, “Hata kama wewe ni jamaa yangu, haifai unifanyie kazi bila ujira. Niambie, mshahara wako utakuwa nini.”

Labani alikuwa na binti wawili, binti mkubwa aliitwa Lea na binti mdogo aliitwa Raheli. Lea alikuwa na macho dhaifu, lakini Raheli alikuwa na umbo la kupendeza na mzuri wa sura. Yakobo akampenda Raheli, akamwambia Labani, “Nitakutumikia kwa miaka saba kwa ajili ya kumpata Raheli binti yako mdogo.”

Labani akasema, “Ni bora zaidi nikupe Raheli kuliko kumpa mtu mwingine yeyote.

Kaa pamoja nami hapa.” Kwa hiyo Yakobo akatumika miaka saba ili kumpata Raheli, lakini ilionekana kwake kama siku chache tu, kwa sababu ya upendo wake kwa Raheli.

Ndipo Yakobo akamwambia Labani, “Nipe mke wangu. Muda wangu umekamilika, nami nataka kulala na yeye.”

Basi Labani akaalika watu wote wa mahali pale na akafanya karamu. Lakini ilipofika jioni, akamchukua Lea binti yake akampa Yakobo, naye Yakobo akalala naye. Kesho yake asubuhi, Yakobo akagundua kuwa amepewa Lea! Basi Yakobo akamwambia Labani, “Ni jambo gani hili ulilonitendea? Nilikutumikia kwa ajili ya Raheli, Sivyo? Kwa nini umenidanganya?”

Labani akajibu, “Sio desturi yetu kumwoza binti mdogo kabla ya kumwoza binti mkubwa. Maliza juma la arusi ya binti huyu, kisha pia nitakupa huyu binti mdogo, kwa kutumika miaka mingine saba.”

Naye Yakobo akafanya hivyo. Akamaliza juma na Lea, kisha Labani akampa Raheli binti yake kuwa mke wake  Pia Yakobo akalala na Raheli, naye akampenda Raheli zaidi kuliko Lea. Yakobo akamtumikia Labani kwa miaka mingine saba.

Kulikuwa na wivu kati ya Lea na Raheli. Lea alikuwa na wivu kwa sababu Raheli alipendwa zaidi na bwana wao. Raheli naye alikuwa na wivu kwa sababu Lea alikuwa na wavulana wengi kabla ya Raheli apate hata mmoja. Mwishowe Raheli alizaa Yusufu na Benyamini. Baada ya kupita muda, Mungu alimbariki Yakobo na wavulana kumi na wawili. Pia, licha ya Labani kujaribu kumdanganya tena na tena, Mungu alimbariki na utajiri.