Katika mwanzo wa vitu vyote, Mungu alipoziumba mbingu na dunia, aliumba mwanamume na mwanamke siku ya sita. Hivi ndivyo alivyofanya!
Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai, mtu akawa nafsi hai. Jina lake lilikuwa Adamu. Mungu pia alipanda bustani maalum iliyoitwa Edeni. Ndani yake alipanda kila aina ya miti mizuri ambayo ilikuwa nzuri kwa chakula. Katikati ya bustani alipanda miti miwili maalum, Mti wa Uzima na Mti wa Ujuzi wa Mema na Mabaya.
Basi Mungu akamchukua mwanamume akamweka ndani ya bustani ailime na kuitunza. Mungu akamwambia, “Ule matunda kutoka kila mti ndani ya bustani, lakini usile matunda kutoka mti uliomo katikati ya bustani uitwao mti wa ujuzi wa mema na mabaya, kwa sababu siku utakayokula hakika utakufa.”
Kisha Mungu akasema, “Si vyema huyo mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.” Mungu akamletea Adamu viumbe vyote vipite mbele yake. Adamu akakipa kila kiumbe jina lake. Lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. Basi Mungu akamletea Adamu usingizi mzito. Alipokuwa akilala, Mungu akatwaa ubavu wake na akafunika pahali hapo kwa nyama. Na kutoka ubavu Mungu akamwumba mwanamke.
Adamu alipoamka, Mungu akamletea mwanamke. Adamu alipomwona yule mwanamke, akasema, “Hatimaye! Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu. Basi, ataitwa mwanamke kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.”
Kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye atajiunga na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. Adamu na mkewe walikuwa uchi wote wawili, wala hawakuona haya.