Kwa zaidi ya miaka mia nne Mungu hakuongea na Wayahudi kupitia manabii.
Kulikuwa kimya kabisa. Pia, Wayahudi walitawaliwa na ufalme wa Rumi. Basi siku moja, Mungu aliongea tena! Alimtuma malaika aliyeitwa Gabrieli kuongea na Zakaria, mmoja wa makuhani hekaluni. Akamwambia kwamba mke wake Elisabeti angemzaa mwana ambaye angetangaza kuja kwa Mwokozi aliyeahidiwa. Zakaria hakuamini kwa sababu yeye na mke wake walikuwa wakongwe na hawakuwa na mtoto. Mungu akamfanya Zakaria kuwa bubu hadi baada ya kuzaliwa kwa mwanawe.. Lakini Mungu alifanya alivyosema. Elisabeti alimzaa mtoto aliyeitwa Yohana. Yeye ndiye alikuwa Mhubiri jangwani kutangaza kuja kwa Mwokozi.
Miezi sita baada ya Malaika Gabrieli kuongea na Zakaria, Mungu alimtuma malaika wake Gabrieli katika mji wa Nazareti, katika nyumba ya bikira aliyeitwa Mariamu.
Mariamu alikuwa ameahidiwa ndoa na mwanamume aliyeitwa Yusufu aliyekuwa wa jamaa ya Daudi.”
Malaika Gabrieli alimwambia Mariamu, “Salamu kwako, uliyebarikiwa na Mungu.
Mariamu alichanganyikiwa na kuogopa. Gabrieli akamwambia, “Mungu amekubariki kwa maana utamzaa mwana. Utamwita Yesu. Atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Mkuu Zaidi. Mungu atampa kiti cha enzi cha babake Daudi naye atatawala juu ya Israeli na Yuda milele.
Yusufu, mchumba wa Mariamu alikuwa mtu wa haki. Alipotambua kwamba Mariamu alikuwa na mimba, hakutaka kumtia aibu mbele ya watu, kwa hivyo alipanga kuvunja ile posa na kumpa talaka katika njia ya siri. Alipokuwa akifikiria kuhusu jambo hilo, malaika wa Bwana alimjia katika ndoto. “Yusufu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Mariamu awe mke wako. Mimba aliyo nayo ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu wa Mungu. Atajifungua Mwana nawe utamwita Yesu maana yake “Bwana anaokoa,” kwa sababu atawaokoa watu wake kutoka kwa dhambi zao. Yusufu alipoamka kutoka kwa ndoto yake, alimchukua Mariamu kama mkewe akampeleka nyumbani lakini hakulala naye hadi alipojifungua.
Miezi sita baada ya Elisabeti kujifungua, Mariamu alikuwa tayari kujifungua pia.
Wakati huo, mfalme wa Urumi alitoa amri kwamba kila mtu anapaswa kurudi katika mji wa jamaa yao, ili kuhesabiwa kwa lengo la ushuru. Yusufu alitoka katika nyumba ya Daudi. Kwa hivyo alirudi Bethlehemu ya Yuda ili kuhesabiwa pamoja na Mariamu, mkewe aliyemposa, aliyetarajia mtoto.
Watu wengi walikuwa wanasafiri ili wahesabiwe kwa hivyo hawakupata pahali pa kukaa katika Bethlehemu. Kwa hivyo walipata pahali pa wanyama. Walipokuwa hapo,
Mariamu alijifungua mtoto wa kiume akamfunga katika nguo za kitoto na kumlaza katika hori ya kulisha ng’ombe.
Karibu na hapo, kulikuwa na wachungaji wakichunga wanyama wao usiku. Punde, malaika akawatokea, na utukufu wa Bwana ukawaangazia, nao wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, “Msiogope. Nawaletea habari njema yenye furaha kuu kwa watu wote. Katika mji wa Daudi, Mwokozi amezaliwa kwenu ambaye ni Kristo Bwana. Hii itakuwa ishara kwenu kumtambua. Mtapata mtoto amefungwa katika nguo za kitoto na amelazwa katika hori ya kulisha ng’ombe.” Halafu, jeshi la malaika likatokea na kuimba, “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”
Malaika walipotoweka, wachungaji waliambiana, “Twendeni Bethlehemu na tuone jambo hili ambalo Bwana alilotujulisha.” Kwa hivyo walienda kwa haraka wakampata Yusufu, Mariamu, na mtoto aliyelala katika hori.
Baada ya kuona Yesu, wachungaji walirudi wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa mambo yote walikuwa wameyasikia na kuyaona na wakaeneza neno hilo kila pahali kuhusu walichoona na kusikia. Na kila mtu aliyesikia habari hii alistaajabu.