Baada ya Mungu kumlaani Kaini, Kaini alipata mke nao wakapata watoto. Sethu naye pia alipata mke nao wakazaa watoto. Baada ya vizazi vingi, watu wakawa wengi ulimwenguni. Watu wengine walimpenda Mungu lakini wengi wao waliasi dhidi ya Mungu. Kila mara walikuwa wakipigana.
Mungu akaona kwamba mawazo yote ya moyo wa mwanadamu yalikuwa maovu wakati wote. Mungu alipoona jinsi kazi za mwanadamu zilivyojaa uovu, alisema, “Nitaangamiza kila kitu nilichoumba, mwanadamu na wanyama pia.”
Kazi ya Nuhu
Lakini Nuhu alipata kibali machoni pa Mungu. Alikuwa mtu mwenye haki aliyetembea na Mungu. Mungu akamwambia Nuhu, “Ninasikitika kwamba niliwahi kumwumba mwanadamu. Nitaangamiza vitu vyote ambavyo vimeumbwa kwa sababu watu wamekuwa waovu, lakini nitafanya agano na wewe. Ni wewe tu, na mke wako, na wanao watatu, na wake wao ambao wataishi.
“Nataka ujenge mashua kubwa inayoitwa safina, kwa sababu nitaleta gharika kubwa itakayoangamiza ulimwengu. Lazima uchukue kila aina ya mnyama na ndege wa kiume na kike. Pia, kwa wanyama ambao wanafaa kwa kutoa dhabihu, lazima uweke wakiume saba na wakike saba. Ulete vyakula pia.”
Mungu alimwambia Nuhu jinsi ya kujenga safina hiyo. Naye Nuhu akafanya yote ambayo Bwana alimwamuru afanye. Nuhu alitumia miaka mingi kujenga mashua hiyo. Siku moja Mungu akamwambia Nuhu kwamba yeye na jamaa wake wachukue wanyama wote na ndege waingie katika safina. Kisha Mungu akafunga mlango uliokuwa mmoja tu.
Mvua na Kusubiri
Kwa siku arobaini na usiku arobaini maji yaliyo juu yalinyesha chini na maji yaliyo chini yalifunguka yakaja juu ya ardhi. Kila kitu kilifunikwa kwa maji hata milima iliyokuwa mirefu zaidi, na hapakuwa na njia kwa watu kuepuka, kwa hivyo wote walizama wakafa maji. Lakini Nuhu na familia yake na wanyama katika safina walikuwa salama, wakielea juu ya maji.
Baada ya siku arobaini Mungu akamkumbuka Nuhu na akasimamisha maji. Kwa miezi mingi Nuhu alikuwa katika mashua. Baada ya mwaka mmoja mafuriko yakarudi chini, safina ikatua juu ya mlima.
Baraka ya Mungu
Kisha Mungu akamwambia Nuhu, “Toka ndani ya safina.” Naye Nuhu, na familia yake, na wanyama wakatoka ndani ya safina. Nuhu akajenga madhabahu na akamtolea Mungu dhabihu akimwabudu. Mungu alipendezwa na dhabihu yake. Mungu akasema, “Kamwe sitauangamiza ulimwengu tena kwa gharika. Ninauweka upinde wa mvua
angani kama ishara ya ahadi yangu.” Mungu akambariki Nuhu na wanawe, akawaambia, “Mkaongezeke, mkaijaze nchi.”
Mungu akamwambia Nuhu, “Sasa ninawapa wanyama kwa chakula. Bali msile damu ya mnyama, kwa sababu ni uhai wake. Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake pia itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu.”
Wana wa Nuhu wakapata watoto wengi na wakati ulipoendelea kupita, kukawa na watu wengi ulimwenguni tena.