CBS Stories

Swahili Stories

Ndama wa Dhahabu

Kutoka 32

Musa alipoenda juu mlimani kuongea na Mungu, Mungu alifanya mbao mbili za mawe na kwa kidole chake akaandika Amri Kumi kwenye mbao hizo. Musa akakaa mlimani kwa siku arobaini.

Watu walipoona kwamba Musa alikawia kushuka mlimani, walikusanyana wakamwendea Haruni wakamwambia, “Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata. Watu wote wakazivunja pete za dhahabu zilizo katika masikio yao, wakamletea Haruni. Akazichukua na akafanyiza sanamu katika mfano wa ndama. Kisha wakasema, “Hiyo ndiyo miungu yako Waisraeli, iliyowatoa katika nchi ya Misri.” Kisha wakaanza kuimba na kucheza na kuiabudu sanamu ya ndama wa dhahabu.

Kileleni mwa mlima, Mungu alikuwa amemaliza kuandika Amri Kumi na akamwambia Musa, “Watu wameshaniasi. Niache ili niwaangamize!” Lakini Musa alimwomba Mungu kukumbuka agano lake na Abrahamu, Isaka, na Yakobo na kutowaangamiza watu wake.

Basi Musa akashuka mlimani. Alipoona watu wakiimba, kucheza, na kuuabudu sanamu ya ndama wa dhahabu, alighadhabika. Akatupa zile mbao za mawe za amri chini nazo zikavunjika vipande vipande. Kisha Musa akatoa sauti kuu akasema, “Kama yeyote anamwabudu Mungu wa kweli, aje kwangu!” Kabila la Lawi tu, ndiyo walimjia. Musa akawaambia, “Kila mtu atwae upanga wake na kuwaua wale wote ambao wanaabudu ndama wa dhahabu.” Watu wengi wakafa na Waisraeli wengine, wakatubu dhambi zao.

Kwa sababu Musa alikuwa ameshavunja zile mbao za mawe za Amri Kumi, alirudi mlimani kwa Mungu. Naye Mungu akatengeneza nyingine. Hizo zilikuwa mbao ambazo Musa aliziweka kwenye sanduku la agano.

Baada ya siku nyingi kwenye Mlima wa Sinai, Mungu aliwaongoza kuelekea katika nchi ya ahadi.