CBS Stories

Swahili Stories

Mwanamke na Nyoka

Mwanzo 3

Nyoka alikuwa mwerevu zaidi katika wanyama wote Mungu aliowafanya. Siku moja, mwanamke alikuwa ndani ya bustani. Nyoka alimwendea akasema, “Ati, hivi ndivyo alivyosema Mungu, ‘Msiyale matunda ya miti yote ya bustani?’”

Mwanamke akamwambia nyoka, “Hapana. Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula, lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema ‘Msiyale wala msiyaguse msije mkafa.’”

Nyoka akasema, “La! Si kweli. Mungu anajua kwamba utakapoyala matunda ya mti huu, utakuwa mwerevu kama yeye.”

Mwanamke akauona mti. Akaona kwamba ulipendeza kwa macho na ulifaa kwa chakula. Na ungesaidia kupata hekima. Kwa hivyo, alilichukua tunda na akalila akampa mume wake aliyekuwa naye, naye akala pia. Punde, macho yao yalifumbuka, wakaona ya kuwa walikuwa uchi. Kwa hivyo walikimbilia msituni na wakatwaa majani kufunika miili yao.

Kujificha

Wakati huo, walimsikia Mungu akitembea katika bustani. Akamwita mwanamume, “Uko wapi?”

Adamu akasema, “Nilikusikia na nikaogopa, kwa hiyo nikajificha kwa kuwa niko uchi.”

Mungu akasema, “Ni nani aliyekuambia kwamba uko uchi? Je, umeyala matunda

kutoka mti ambao nilikuagiza usile?”

Adamu akasema, “Huyu mwanamke uliyenipa alinipa tunda nami nikala.” Kisha Mungu akamwambia mwanamke, “Umefanya nini?”

Mwanamke akasema, “Nyoka amenidanganya nami nikala.”

Laana, Rehema, na Utengano

Basi Mungu akamwambia nyoka, “Kwa sababu ya yale umefanya, umelaaniwa!

Utatambaa kwa tumbo lako kwa siku zako zote. Utakula mavumbi ya ardhi. Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.”

Kisha Mungu akamwambia mwanamke, “Kwa sababu ya yale umefanya, umelaaniwa! Utakuwa na uchungu unapozaa. Tamaa yako itakuwa dhidi ya mumeo, naye atakutawala.”

Kisha Mungu akamwambia Adamu, “Kwa sababu umemsikiliza mkeo na hukunisikiliza, wewe pia umelaaniwa na nchi imelaaniwa kwa sababu yako! Utafanya kazi ngumu siku zote za maisha yako ukitoa jasho, na miiba na mimea isiyofaa itakua. Kisha utakufa! Utarudi mavumbini ambamo ulitwaliwa.”

Wakati huo, mwanamume akampa mwanamke jina jipya. Akamwita Hawa, kwa kuwa yeye ndiye alikuwa mama yao wote walio hai.

Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi akawavika.

Kisha Mungu akasema, “Mtu huyo sasa amekuwa kama mmoja wetu kwa kujua mema na mabaya. Sharti asiruhusiwe kuchukua matunda ya mti wa uzima na kula na kuishi milele.” Kwa hivyo Mungu aliwafukuza kutoka bustanini, kisha akamweka malaika na upanga wa moto uliogeuka huko na huko kuilinda njia ya mti wa uzima.