CBS Stories

Swahili Stories

Kuvuku Bahari ya Shamu

Kutoka 13:17-14:31

Kutembea Jangwani / Kunaswa!

Baada ya Mungu kuwakomboa wana wa Israeli kutoka Misri, badala ya kwenda njia iliyo karibu sana na Kanaani, aliwaongoza kupitia jangwani mpaka Bahari ya Shamu. Wakati wa mchana, Mungu aliwaongoza kwa nguzo ya wingu na usiku katika nguzo ya moto ili kuwapa mwanga wa kuona.

Lakini Farao aliposikia kwamba waliondoka, alibadilisha mawazo yake tena. “Tumefanya nini? Tumewaachilia watumwa wetu!” Kwa hivyo Farao alilichukua jeshi lake na magari ya farasi wake na wakawafuata Waisraeli. Wakawafikia katika Bahari ya Shamu. Waisraeli walitegwa baina ya jeshi na bahari. Hawakuweza kutoroka.

Watu walipowaona Wamisri, waliwaogopa sana. Wakamwuliza Musa, “Musa, kwa nini umetuleta hapa jangwani kufa? Je! hili silo tulilokuambia huko Misri: ‘Utuache ili tuwatumikie Wamisri’? Kwa maana ingekuwa heri kwetu kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani.”

Msimame Imara! / Gawanya Bahari na Kuvuka!

Musa akawajibu watu, “Msiogope. Simameni imara! Nanyi mtaona ukombozi ambao BWANA atawaletea leo. Wamisri mnaowaona leo, hamtawaona tena. BWANA atawapigania ninyi; mnahitaji tu kutulia.” BWANA akanena na Musa, na kumwambia, “Mbona unanililia? Waambie watu wasonge mbele! Inua fimbo yako juu ya bahari, ili kuyagawanya maji, ili watu wavuke kwenye nchi kavu. Nami nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao watakufuata, nami nitajipatia utukufu kwao; nao Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.” Wakati huo Bwana akasogea nyuma yao katika nguzo ya wingu ili kuwalinda na jeshi la Wamisri. Usiku kucha lile wingu lilileta giza kwa Wamisri na mwanga kwa Waisraeli. Kwa hivyo Musa alinyoosha fimbo yake na Mungu akafanya bahari irudi nyuma kwa nguvu za upepo mkali. Maji yaligawanyika na Waisraeli wakavuka kupitia ndani ya bahari kama kupitia juu ya nchi kavu, kukiwa na ukuta wa maji kulia na kushoto. Farasi na magari yote ya Farao yaliwafuata ndani ya bahari.

Ukombozi

Usiku ulipokaribia kwisha, Mungu aliangalia jeshi la Misri na akalifanya kuchanganyikiwa. Akafanya magari yao yapoteze magurudumu yao, na kuwa vigumu kuyaendesha. Wamisri wakasema, “Tuwaache Waisraeli peke yao. Bwana anawapigania dhidi yetu.”

Basi Mungu akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi juu ya Wamisri.” Kisha bahari ikarudi pamoja na kuwaangamiza Wamisri wote. Hakuna hata mmoja ambaye alitoroka.

Siku hiyo, Mungu aliwaokoa Waisraeli dhidi ya Wamisri. Kesho yake alfajiri wakawaona Wamisri wakiwa wamekufa ufukoni mwa bahari. Walipoona uwezo mkuu wa Mungu, walimcha Mungu, na wakamtumaini. Na pia, wakamtumaini mtumishi wake Musa.