Baada ya Mungu kuwafukuza Adamu na Hawa kutoka bustanini, Hawa alipata mimba na akamzaa mwana. Wakamwita mvulana huyo Kaini. Baadaye, Hawa alimzaa mwingine aliyeitwa Habili. Kaini alipokua akawa mkulima. Habili naye alipokua akawa mchungaji wa wanyama.
Siku moja wote wawili walimletea Mungu dhabihu. Kaini alileta sadaka kutoka shambani mwake baadhi ya matunda na mboga. Habili naye alileta sehemu nono ya wazaliwa wa kwanza wa kondoo wake. Alizitoa kama dhabihu na damu ilimwagika.
Mungu aliikubali dhabihu ya Habili lakini hakuikubali dhabihu ya Kaini. Kaini alighadhabika sana. Mungu akamwuliza Kaini, “Kwa nini umekasirika? Ukifanya yaliyo mema, je, hutakubalika? Lakini ukifanya maovu, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, inakutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.”
Baadaye Kaini akamwambia kakake Habili, “Twende uwanjani.” Walipokuwa wakitembea uwanjani, Kaini alimwua Habili, kisha akaenda zake.
Baada ya mkasa huo, Mungu akamwuliza Kaini, “Kaka yako Habili yuko wapi?” Kaini akasema, “Sijui. Je, mimi ndimi humtunza?” Kisha Mungu akasema, “Damu ya kakako inanililia kutoka ardhini! Umelaaniwa! Nchi haitakutolea mazao. Lazima uondoke pahali hapa na kuzurura huku na huko duniani.”
Kaini akasema, “Aaa, jambo hili ni gumu sana kwangu, umenifukuza kutoka duniani. Umenifukuza kutoka uwepo wako, na yeyote atakayeniona ataniua.”
Kisha Mungu akaiweka alama kwa Kaini na akasema, “Yeyote atakayemwua Kaini nitamlipiza mara saba.”
Kisha Kaini akaondoka akazurura huku na huko. Baadaye Kaini alipata watoto.
Walikuwa waovu na hawakumwabudu Mungu.
Nao Adamu na Hawa wakapata mwana mwingine aliyeitwa Sethu mahali pa Habili aliyekufa. Lakini wengi wa familia ya Sethu walimwabudu Mungu.